LIJUE BARAZA LAKO-BAKWATA

BARAZA KUU LA WAISLAMU WA TANZANIA - BAKWATA NATIONAL MOSLEM COUNCIL OF TANZANIA المجلس الأعلى للشئون الإسلامية بتنزانيا

Monday, July 10, 2006

Bakwata yafukuza viongozi wake saba

Bakwata yafukuza viongozi wake saba!
31 Mar 2006

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limewatimua kazi viongozi wake saba baada ya kubainika kuwa, waliingia mikataba `feki` ya uuzwaji wa kiwanja cha Waislamu, eneo la Chang`ombe, jijini Dar es Salaam. Hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Shaaban bin Simba. Sheikh Mkuu aliwataja viongozi hao waliofukuzwa kuwa ni Katibu Mkuu Ustadhi Abbas Kihemba, N aibu Katibu Mkuu upande wa dini Sheikh Mussa Hemed, Ustadhi Rajabu Ndewa, Wadhamini wa Bakwata Alhaj Seif Momba na Seif Swai,Imamu wa Msikiti wa Farouk ulio BAKWATA makao makuu, Sheikh Ally Mbaraka na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya taifa ya BAKWATA Alhaj Seleman Mwenda. Sheikh Mkuu alisema, BAKWATA ilifikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya Tume aliyoiunda kufuatilia sakata hilo ili kubaini ukweli. Alisema ripoti ya Tume hiyo iliyokuwa imeundwa na watu watano, ilibaini kuwa, kiwanja kilichokuwa kikileta ugomvi ni mali ya BAKWATA na kwamba viongozi wao walifanya ulaghai huo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Aidha, Sheikh Mkuu aliiomba serikali kuingilia kati ili kukirudisha kiwanja hicho kwa Waislamu kwa kuwa imebainika kuwa ni mali yao. Alisema kiwanja hicho kilifanyiwa hujuma tangu mwaka 1984 na serikali haina budi kukirudisha kama kilivyokuwa. Alisema wakati wa uuzwaji wa kiwanja hicho, zilitumika nembo za BAKWATA ili kuonyesha kuwa wamehusika na mpango huo jambo ambalo sio kweli. Uuzwaji wa kiwanja hicho ulizua mtafaruku mkubwa hali iliyosababisha kuitishwa kwa maandamano makubwa yaliyohusisha waumini wa dini ya Kiislamu. Kiwanja hicho kinadaiwa kuuzwa kwa kampuni ya Quality Group ya jijini Dar es Salaam inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Bw.Yusuph Manji. Aidha, kiwanja hicho hivi sasa kimedaiwa kujengwa shule pamoja na majengo mengine na kubaki sehemu ndogo. Mufti alisema kuwa Tume hiyo itaendelea na kazi ya kufuatilia mali za Waislamu zilizoporwa na taasisi ama watu binafsi kwa nchi nzima.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home