LIJUE BARAZA LAKO-BAKWATA

BARAZA KUU LA WAISLAMU WA TANZANIA - BAKWATA NATIONAL MOSLEM COUNCIL OF TANZANIA المجلس الأعلى للشئون الإسلامية بتنزانيا

Monday, July 10, 2006

Bakwata yachunguza msikiti kuvunjwa

Bakwata yachunguza msikiti kuvunjwa
Written by Muhibu Said
Wednesday, 05 July 2006

BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), linachunguza ukweli wa hatua ya kuvunjwa kwa Msikiti wa Aqram uliopo eneo la Shabaha, Mbezi jijini Dar es Salaam unaodaiwa kuvunjwa na vijana wapatao 40 wakishirikiana na polisi saba wa kituo cha Kawe.
Naibu Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, aliliambia Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa, Bakwata imefikia uamuzi huo ili kubaini ukweli wa tukio hilo kabla ya kuchukua hatua.
Sheikh Zubeir alisema uamuzi wa kuchunguza tukio hilo ulifikiwa katika kikao cha Baraza la Ulamaa la Bakwata kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam chini ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa Bin Shaban Simba.
"Tumeona tusiridhike tu na taarifa za vyombo vya habari, ni vizuri kwanza tufanye uchunguzi kabla ya kutoa tamko," alisema Sheikh Zubeir.
Msikiti huo uliovunjwa Mei 31, mwaka huu, ulikuwa kwenye kiwanja chenye mgogoro kati ya Waislamu wa eneo hilo na mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake, anayedaiwa kumiliki nyumba tatu tofauti kwenye eneo hilo.
Msikiti huo unadaiwa kuwa ulikuwa na uwezo wa kuchukua waumini 150.
Imamu wa Msikiti huo, Sheikh Saidi Juma, alikaririwa na gazeti hili akisema kiwanja hicho kilikuwa na mgogoro wa takriban miaka mitatu na kuwa mtu mmoja aliwapeleka Waislamu katika Mahakama ya Kinondoni ambako kesi iliendeshwa kinyemela na hukumu kutolewa Machi 20, mwaka huu.
Hata hivyo, Sheikh Juma, alidai kuwa walijenga msikiti huo kwa ruhusa ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home