LIJUE BARAZA LAKO-BAKWATA

BARAZA KUU LA WAISLAMU WA TANZANIA - BAKWATA NATIONAL MOSLEM COUNCIL OF TANZANIA المجلس الأعلى للشئون الإسلامية بتنزانيا

Monday, July 10, 2006

Bakwata kufanyiwa marekebisho makubwa
2006-06-17 13:31:37

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba, ameahidi kulifanyia mabadiliko makubwa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA) ili liweze kuwanufaisha Waislamu wote nchini. Aliyasema hayo jana baada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtoro, Jijini Dar es Salaam. Alisema kumekuwapo na malalamiko mengi yanayowahusu baadhi ya viongozi wa baraza hilo na aliahidi kuchukua hatua za kulisafisha. Alisema baraza hilo ni la wote na kwamba linapaswa kuwanufaisha Waislamu wote. Aliwataka waumini wa Msikiti huo na Waislamu wote nchini walitambue kuwa, ni lao na si la kundi fulani. Hata hivyo, alisema ni vigumu kulisafisha kabisa na kuwa na watu safi kwa kuwa wanadamu wanabadilika wakati wowote. ’’Kusafisha binadamu ni kazi kubwa, leo utaweka huyu ataharibu utaweka huyu yale yale lakini tutajitahidi kusafisha tubaki na watu wanaowatumikia Waislamu,’’ alisema. Alisema Waislamu popote walipo wanawajibu wa kwenda kutoa maoni yao kuhusu utendaji wa baraza hilo na kwamba kwa kufanya hivyo watasaidia kwa kiasi kikubwa. ’’Njooni kwa wingi tukosoane tutarekebishana hivyo hivyo’’, alisisitiza na kuahidi kuwa milango ya baraza hilo iko wazi kwa waumini wa dini hiyo. Alisema alishaanza kufanya mabadiliko mara baada ya kusikia malalamiko ya Waislamu kuwa ndani ya Baraza hilo kuna watu wanafanya kazi kwa maslahi yao na si ya waislamu. Kuhusu elimu alisema Uislamu unahitaji elimu na kwamba jitihada zinahitajika kwa kiasi kikubwa kuwainua waislam kielimu. Alisema hivi sasa BAKWATA ina shule 20 tu za sekondari nchini ambazo alisema haziwezi kutosheleza mahitaji yao ya kielimu. Alisema kunahitajika nguvu za pamoja kujenga vyuo na shule za sekondari na kwamba endapo watakuwa kitu kimoja suala hilo linawezekana. ’’Tukijichangisha Waislamu wote tunaweza kufanya makubwa tatizo lililopo hatuko kitu kimoja kama familia, sasa utengano na makundi yasipewe nafasi tuwe wamoja’’, alisisitiza. Sheikh Mkuu aliwapongeza waumini wa msikiti huo kwa kuwa mstari wa mbele kupigania haki mali na haki za Waislamu nchini. Alisema Katiba ya baraza hilo ni nzuri na iko kwa maslahi ya wote tofauti na hisia ya baadhi ya waislamu kuwa inapendelea wa kundi fulani. Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti huo, Sheikh Hamis Khalifa, alisema awali walikuwa na kawaida na kutoliamini baraza hilo lakini hivi sasa wameanza kuwa na imani nalo. Alisema walikuwa wakielezea matatizo yao ikiwa ni pamoja na kuporwa kwa mali za waislamu lakini hakukuwa na kiongozi aliyechukua hatua. ’’Kule ndani ya BAKWATA kulikuwa na watu wanajifanya watawala wa Waislamu na si viongozi lakini tunakushukuru kwa kuunda kamati ya kuchunguza madai yetu, ’’ alisema. Alimshauri Sheikh Mkuu kupita kila mkoa na kuzungumza na Maimamu wa mikoa ili wamweleze kero za waislamu. ’’Kwanza tunakushukuru kwa kuwa haijapata kutokea Msikiti huu kutembelewa na Mufti hii ni nafasi ya pekee’’, alisema Sheikh Khalifa.
SOURCE: Nipashe

0 Comments:

Post a Comment

<< Home